WELCOME !

THANK YOU FOR VISITING THIS SITE. I HAVE BEEN USING BOTH SWAHILI AND ENGLISH LANGUAGE TO EXPRESS ISSUES - I HAVE ATTACHED ENGLISH VERSION TO SOME OF THE SWAHILI NEWS/STORY AT THE END.

Thursday 20 October 2016

UHALIFU MTANDAO UNATEGEMEWA KUKUA ZAIDI MAENEO MENGI

Takwimu za uhalifu mtandao zimeendelea kukua huku wana usalama mtandao wakiendelea kutafuta suluhu ya kudumu dhidi ya uhalifu mtandao maeneo mengi duniani. Hivi sasa tumefikia wakati wa kila tunavyotumia ku unganishwa kwenye mtandao (Internet of Things – IoT) ambapo Televisheni, Friji , Majiko, Magari na kadhalika vimekua vikiunganishwa mtandaoni ili kurahisisha maisha ya watumiaji.

Hali hii imepelekea wimbi kubwa la uhalifu mtandao kuendelea kukua na imetabiriwa kadri muda unavyoendelea tishio la uhalifu mtandao litakua kubwa zaidi – Kuliangalia hili Mkutano wa wana TEHAMA wa Nchi za Afrika (AfICTA) wa mwaka huu 2016 ambao uliofanyika jijini Windhoek Nchini Namibia ulipata kujadili mengi kuhusiana na hili ambapo pande mbili za faida na changamoto ziliangaziwa kwa karibu.

Binafsi, Nilipata kushiriki kuongoza mijadala miwili ambapo tuliangazia changamoto za ukuaji wa uhalifu mtandao kutokana na wimbi wa vitu vingi kuendelea kuunganishwa mtandaoni na pia kujadili mapendekezo ya mambo ya msingi ya kuzingatia ili kubaki salama pamoja na mambo ya msingi kwa wadhibiti wa uhalifu mtandao wanayopaswa kuzingatia ili kuweza kudhibiti hali hii.

------------------------------------------------------------
HABARI NJEMA: Nimeteuliwa kua Mjumbe wa bodi ya wana TEHAMA wa Nchi za Afrika (AfICTA) ambapo nitaungana na wajumbe wengine kusukuma gurudumu la TEHAMA katika Nchi za Afrika na Dunia Kwa Ujumla – Kujua zaidi kuhusiana na wajumbe wote wa Bodi Unaweza kusoma kwa “KUBOFYA HAPA”
------------------------------------------------------------

Mjadala ulisistiza ya kua wahalifu mtandao hawapaswi kutuzidi nguvu na kuturudisha nyuma ila kinacho paswa ni kujipanga zaidi kwa kuwekeza katika ulinzi mtandao ili kulinda wimbi la vifaa vinavyoendelea kuunganishwa mtandaoni dhidi ya wahalifu mtandao.


Napenda nitoe mfano mdogo kwenye mfumo wa kifedha Tanzania – Hivi sasa malipo ya takriban kila kitu yameunganishwa mtandaoni ambapo wananchi wanaweza kulipa bili, kufanya miamala ya kufedha na hata kuhamisha fedha kutoka kwenye mfumo mmoja kwenda mwingine kupitia mtandao na simu za viganjani.

Hii inamaana kwamba, Mfumo unganishi wa haya yote unapopata itilafu ya kuingiliwa na wahalifu mtandao unaweza situ kusababisha usumbufu kwa watumiaji bali unaweza kupelekea hasara kubwa kwa Taifa.

------------------------------------------------
HABARI: Mchango wangu katika sekta ya Usalama mtandao barani Afrika na Duniani kwa Ujumla umezaa matunda na kwa mara ya kwanza nimeweza kutunukiwa tunzo kubwa ambapo nimeweza kuiandikia kwa kirefu “HAPA”
------------------------------------------------

Tumeshuhudia taarifa za angalizo juu ya Uhalifu mtandao kwa Mwezi wa Kumi zilizizo kua zikisambaa mitandaoni na baadae kuona mashambulizi mtandao katika baadhi ya Tovuti Nchini kitu ambacho kimekua cha kushangaza – Kwanini Hatua hazikukuchukuliwa mapema kabla ya kutokea wakati tayari angalizo lilitolewa? Na hii si mara ya kwanza.

Hii inaonyesha bado utayari wetu kama Taifa unavyo onekana kusua sua – Hili si tatizo la kwetu pekee, Mataifa mengi hasa barani Afrika yameendelea kukumbwa na matukio mfano wa hili ambapo angalizo linakuja kabla lakini panakua hakuna hatua stahiki hadi pale matukio yanapo tokea.

Kufuatia hili ndilo lililopelekea binafsi kuwaeleza washiriki katika mkutano ulio kamilika Nchini Namibia ya kua lazima ifike mahali tuwe tuna fikiri na kufanya vitu tofauti na mazoea – Na kubwa zaidi lazima tujipange kwenye udhibiti badala ya kutafuta suluhu baada ya tatizo kutokea. Ukiangalia andiko linaloweza kusomeka “HAPA” nimefafanua zaidi hili.

Aidha, Kumekua na mapendekezo ya msingi ambayo kwa sasa tayari yana na maelekezo ya namna bora yakuyaendea mpendekezo hayo lakini bado kumekua na ugumu kufikiwa malengo hasa  Barani Afrika. Nchi nyingi zimeendelea kufanyia kazi ingawa bado malengo yamekua yakifikiwa kwa shida sana katika kila pendekezo.

Nitoe mfano kwenye hili; Moja ya pendekezo ni elimu ya Uelewa “Cybersecurity awareness programs” ambapo inatakiwa kutolewa kwa watumiaji mtandao – Na kuliwekea hili msisitizo kila mwezi wa kumi (October) Nchi nyingi duniani zimekua zikiadhimisha mwezi huu kama mwezi maalum wa kukuza uelewa kwa watumiaji mtandao (Cybersecurity Awareness month).

Bahati mbaya sana elimu hii ya uelewa imekua ikitolewa bila mafanikio kutokana na kutofata maelekezo yaliyotolewa ili kuweza kutoa elimu inayoweza kua na mafanikio chanya. Pesa nyingi zimeendelea kutumiwa kwenye hili na kila inapofanywa tathmini inaonekana bado wananchi wanakua hawajaelewa.

Mara kadhaa, Nimeshauri kwa wenye dhamana kwenye hili bila mafanikio – Kitu ambacho kinafanya nijiulize tatizo liko wapi? Elimu ya uelewa ambayo nimeweza kutolea mfano wenzetu katika mataifa mengine wanavyo iendea bila kutumia gharama na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa inakuaje tunashindwa?

Jambo jingine nililo sisitiza kwenye mjadala ni kuwaeleza washiriki ya kua ifike mahali tatizo la uhalifu mtandao lionekane kua ni changamoto kubwa na kila mmoja kuanzia ngazi ya mtu binafsi – Kampuni/Shirika – Na Hatimae taifa kwapamoja tuchukue hatua ili kwa pamoja tushinde katika vita hii dhidi ya uhalifu mtandao.

UFAFANUZI: Ngazi ya Mtu binafsi, Kila mmoja lazima ajue ana jukumu la kuhakiki anabaki salama kwa kufanya mambo ya msingi. Mfano,  kua na neno lasiri madhubuti na kufata maelekezo mengine yanayotolewa kwa mtu kujilinda awapo mtandaoni dhidi ya wahalifu mtandao.

Ngazi ya kampuni/Shirika, Kila kampuni au shirika linapaswa kujua linajukum la kuhakiki linalinda taarifa/fedha n.k zake na za wateja wake kwa kua na kitengo maalum chenye utayari na watu wenye uwezo wa kudhibiti uhalifu mtandao. Nchi nyingi ikiwa ni pamoja Nchi za barani Afrika zimeendelea kulifanyia kazi hili na mafanikio yanaonekana.

Ngazi ya Taifa, Kila taifa lazima kuwe na mikakati endelevu kwa kufata maelekezo yanayotolewa na wataalam wa usalama mtandao. Mfano, kua na sheria mtandao (Tanzania tuko vizuri kwenye hili ingawa Nchi nyingi Afrika bado zinasua sua) Kua na kitengo kimoja maalum kwa kinacho angazia ulinzi mtandao katika ngazi ya kitaifa. (Mfano Nchi ya Singapore (Cybersecurity Agency) na mataifa mengine ambapo kumekua hatua nzuri katika kuliendea hili.


Mapendekezo yote na ufafanuzi wake nimekua nikiyaandikia katika maandiko mbali mbali ambapo yanaweza kupitiwa kwa kuangalia taarifa zilizopita. Inakua vigumu kuyaweka yote kwenye andiko hili maana nimeandikia katika maandiko kadhaa tofauti na kuyafafanua ili iwe rahisi kwetu kuweza kuyafata na hatimae kufikia malengo.

No comments:

Post a Comment